Mateso, maumivu na siasa ni mambo yaliyojaa uchochezi mkali unaomsukuma mshairi kuzungumza waziwazi na kinagaubaga na hatimaye kumfanya mwandishi apandwe na jazba zinazofanya kazi fulani itoke nje ya kingo za ulingo wa kisanaa. Katika hali kama hii mshairi lazima atunge wimbo unaoimbika ndani ya nafsi yake mwenyewe kwanza, wimbo utakaomwezesha kunyanyuka kitandani asubuhi huku akijua hayuko pweke, ana wenzake wenye maumivu kama au kuliko yake. Mohammed Khelef Ghassani ana weledi huu wa kubaki ndani ya kingo za ulingo wa kisanaa, weledi wa kuichenga siasa kwa namna ya kuipa nguvu kubwa zinazoficha na kuzimua unagaubaga na hata ukali wake.